Wahitimu wa SUA waongoza kwa kutoa ajira kwa vijana wengine nchini

Mkuu wa wilaya ya Malinyi Mathayo Maselle amekipongeza na kukishukuru Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa kuzalisha wahitimu ambao wanajiajiri na kusaidia kuanzisha miradi ambayo inachangia kutoa maarifa na kuzalisha ajira kwa vijana wengine nchini.

SUA

Mkuu wa wilaya ya Malinyi Mathayo Maselle akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi wa ufugaji wa nyuki wa kisasa kwa vijana wa Wilaya za Ulanga na Malinyi. Kushoto ni Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro Dkt. Rozalia Rwegasira

Mheshimiwa Maselle ambaye alisoma shahada ya kwanza na ya pili SUA amezungumza hayo wakati wa hafla ya uzinduzi wa mradi wa ufugaji wa nyuki wa Kisasa kwa vijana 1500 kutoka wilaya ya Ulanga na Malinyi  unaoendeshwa na kampuni ya ACLA HONEY chini ya program ya kuwajengea ujuzi vijana (SET) inayotekelezwa na Shirika la Swisscontact kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Uswis SDC .

“Mimi nakipongeza sana na kukishukuru Chuo Chetu Cha Sokoine cha Kilimo maana kinatoa mchango mkubwa sana kwenye maendeleo ya nchi hii hasa kwenye eneo la Kilimo, Mmesikia vijana hawa wa ACLA HONEY wanatoka SUA kupitia taasisi ya SUGECO, nakumbuka wakati SUGECO inaanzishwa nilikuwa pale nasoma pia, kwahiyo kazi za vijana wa SUA zinafaida kubwa sana kwa taifa hili mfano mzuri ni huu mradi ambao wahitimu hawa wa SUA wameuleta wilayani kwetu kwaajili ya kusaidia vijana wenzao na kupitia fursa hiyo vijana wanakwenda kujiajiri na kutengeneza uchumi huku halmashauri ikienda kupata mapato” Alisisitiza Mhe. Maselle.

Aliongeza “Vijana waitumie hii fursa, ni fursa muhimu sana ambayo haichoshi kwakuwa unaweza ukaifanya huku ukiwa unafanya shughuli zako nyingine, ukishakuwa na mzinga wako na ukajua mahali pa kuuweka, nenda kauweke pale halafu kaendelee na shughuli zako za shamba huku ukisubiri kwenda kuvuna asali”.
Aidha amewataka vijana waliopata fursa hiyo na wananchi wote waliopata taarifa kuzitumia vizuri fursa zilizopo za misitu Pamoja na kutunza maeneo ili kuweza kufaidika na fursa hiyo ya uvunaji wa nyuki.

Aidha Maselle ameongeza kuwa akiwa kama mmoja  kati ya wahitimu wa SUA, anaunga mkono juhudi hizo zilizoletwa na ACLA HONEY huku akihakikisha matokeo ya kile ambacho kimekusudiwa yanaonekana ili mradi huo ambao ni wa majaribio ufanye vizuri wapate mradi mkubwa wa miaka minne.



Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Kampuni ya ACLA HONEY, Giovanni Nguvu akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo

Akielezea taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Muwakilishi wa Mkurugenzi wa Kampuni ya ACLA HONEY,  Giovanni Nguvu amesema kampuni hiyo ambayo imetokana na wahitimu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kupitia taasisi ya SUGECO ina mashamba kwenye Mikoa saba ya Tanzania yenye mizinga 7,000 na kampuni yao huzalisha asali tani zaidi ya 25,000 kwa mwaka na soko kubwa la asali yao ni nje ya nchi.

Alisema kutokana na uzoefu wa kampuni hiyo na uaminifu, wamekuwa wakitekeleza miradi mbalimbali nchini na sasa wamepata ufadhili wa kutekeleza mradi huu ambao utahusisha wilaya mbili za Malinyi na Ulanga na utawafikia vijana 1500 moja kwa moja wenye umri kati ya 14 hadi 24 na kati yao 5000 wakitoka wilaya ya Ulanga na 1000 wakitoka Wilaya ya Malinyi.

“Mradi huu una malengo ya kukuza kipato cha kaya na kuongeza lishe kupitia ufugaji wa nyuki wa kisasa ambapo pamoja na wanufaika kuunganishwa kwenye vikundi na kupatiwa mafunzo lakini pia watapewa mizinga ya kisasa ya ufugaji wa nyuki,vifaa vya kurina asali na mazao mengine ya nyuki na kuhakikishiwa soko la mazao yote ya nyuki yatakayozalishwa” alieleza Nguvu.

Nguvu ameongeza kuwa mafunzo hayo pia yatakwenda mbali zaidi kwa kuwafundisha mbinu bora za kuongeza thamani mazao yatokanayo na nyuki kama vile kutengeneza Mishumaa, ving’arisha viatu, ving’arisha Midomo, Mvinyo pamoja na bidhaa zingine nyingi.



Viongozi mbalimbali wakifuatilia maelezo ya ufugaji bora wa nyuki na kujionea vifaa vya kisasa vya ufugaji vilivyotolewa kwa ajili ya mradi huo wa ACLA HONEY

Amesema Mradi huo kwa sasa upo kwenye hatua za majaribio kwa kipindi cha miezi saba  kutoka mwezi wa nane  hadi wa tatu mwakani na pindi mfadhili atakaporidhishwa na matokeo ya utekelezaji ya mradi huo, mradi huo utaanza kutekelezwa kwa awamu ya miaka minne ya  Mradi kuanzia Mwezi Mei 2022 hadi mwezi Aprili 2026.

Akizungumza kwa niaba ya vijana wanufaika wenzake wa mradi huu, Faraji Mbowela ameshukuru kwa Shirika hilo kupeleka mradi huo kwenye wilaya yao kwani utawakwamua vijana wengi wanaokaa vijiwemo na wengine kujishughulisha na vitendo hasi kwenye jamii kama vile wizi na uvutaji wa bange.

“Kilichonivutia ni maelezo ya ufugaji wa nyuki na namna biashara hiyo inavyofanyika kwa urahisi tofauti na nilivyokuwa nafahamu lakini pia kuna maslahi makubwa hasa kama mimi natarajia kuwa na familia yangu huko mbeleni hivyo nitahakikisha nafanya kazi kwa bidii kwa kuongeza mizinga kila mara ili nipate asali nyingi zaidi na kuongeza kipato changu” alisema Mbowela

Kushoto ni muhitimu wa Shahada ya Usimamizi wa Utalii kutoka SUA Ellice Mrindoko na kulia ni mmoja wa maafisa wa kampuni ya ACLA HONEY Bw. Godfrey  Rwechungura wakitoa maelekezo kwa mdau kuhusiana na ufugaji bora wa nyuki

Story by
Amina Hezron, SUAMEDIA

Share this page