SUA yapongezwa kwa kutoa elimu ya Kujiajiri kwa Vijana

Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA kimepongezwa kwa kutoa elimu bora nchini inayofundishwa zaidi kwa vitendo ambayo inamjenga Mwanafunzi anapomaliza Chuo aweze kujiajiri na kujitegemea ili kuleta maendeleo kwenye Jamii.

SUA

Jaji Mstaafu Mhe. Joseph Sinde Warioba

Pongezi hizo zimetolewa na Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Jaji Mstaafu Mhe. Joseph Sinde Warioba Siku ya Jumanne tarehe 26 Oktoba, 2021 wakati akizungumza na Menejimenti na wafanyakazi wa SUA katika ukumbi wa Multpurpose Kampasi ya Edward Moringe. 

“Katika miaka 5 niliyofanya kazi SUA nimeona vijana wengi waliomaliza masomo yao hapa wamefungua miradi yao wenyewe na hata wale niliowaona kwenye kituo cha ATAMIZI nina hakika watakuwa mfano mzuri kwenye jamii wakienda kuyatumia mafunzo yao vizuri” alisema Mhe. Warioba.



Jaji Warioba amesema kuwa wakati ameteuliwa kuwa Mkuu wa Chuo hicho mwaka 2016 kulikuwa na changamoto mbalimbali zilizokuwa zinakikabili Chuo kama uchache wa madarasa, uchakavu wa nyumba za watumishi, upungufu wa vifaa, miundo mbinu mibovu ya barabara, ubovu wa viwanja vya michezo na uchache wa wanafunzi.

“Nishukuru sana Menejimenti, Baraza la Chuo na Wafanyakazi wote kwa kufanya kazi kwa bidii na ushirikiano mliouonesha ndio umesaidia kufanya maboresho ya vitu vyote hivi licha ya kuwa na bajeti ndogo ya fedha” alisema mhe. Warioba 

Akitoa neno la utangulizi, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Prof. Raphael Chibunda amemshukuru sana Mkuu wa Chuo hicho kwa ushirikiano wake, ushauri na Miongozo aliyokuwa akiitoa katika kukiongoza Chuo tangu alipoteuliwa kuwa Mkuu wa Chuo hicho.

“Mkuu wa Chuo tunakushukuru sana kwa kipindi cha miaka mitano, tangu ulipoteuliwa umekitembelea Chuo chetu mara 12, umetembelea Kampasi ya Edward Moringe, Kampasi ya Olmotonyi, na kampasi ya Mizengo Pinda pia  umehudhuria mahafali ya Chuo chetu mara tano na kutunuku shahada kwa wahitimu wet una umefanya teuzi mbalimbali. Haya ni machache niliyoyaelezea hakika umefanya mengi” alisema Prof. Chibunda

Profesa Raphael Chibunda

Akizungumzia mafanikio yaliyopatikana katika miaka mitano ya uongozi wa Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Chibunda amesema kuwa idadi ya wanafunzi imeongezeka mpaka asilimia 70, programu za masomo zimeongezeka, kufunguliwa kwa Kampasi ya Mizengo Pinda, maboresho ya miundo mbinu ya kufundishia kama shamba darasa, ununuzi wa mtambo wa kutotolesha vifaranga vya Samaki na ukarabati wa barabara za ndani ya Chuo 

Pia Chuo kimeweza kutekeleza miradi 18 ya maendeleo kwa kujenga na kukarabati madarasa, maabara, karakana za uhandisi, ofisi, nyumba za wafanyakazi, kafeteria ya wanafunzi na maktaba.

“Mkuu wa Chuo, nikushukuru sana kwa sababu wakati unateuliwa kama kulikuwa na sehemu ambayo ilikuwa na upungufu basi ni eneo la kufundishia wahandisi wa kilimo. Kupitia uongozi wako tumeweza kujenga karakana nne ambazo tayari tumeshaagiza vifaa” alisema Prof. Chibunda

Aidha ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais mhe. Samia Suluhu Hassan kupitia wizara ya elimu kwa kutenga fedha kwa lengo ya kusaidia Taasisi za elimu ya juu na Chuo cha SUA kimekuwa ni kimojawapo ambacho kimepata fedha kiasi cha bil. 74.2 kwaajili ya upanuzi wa majengo na kuboreshea miundo mbinu ya Chuo.

Awali akimkaribisha mgeni rasmi, Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo, Jaji Mstaafu Mhe. Mohamed Othman Chande ameshukuru uongozi, Menejimenti, wafanyakazi na baraza la Chuo kwa ushirikiano waliouonyesha kwa Mkuu wa Chuo kwa kipindi chote alichokiongoza.

Akizungumzia mafanikio yaliyopatikana kutoka kwenye Baraza la Chuo katika miaka mitano ya awali ya uongozi wa Mkuu wa Chuo, Mheshimiwa Jaji Chande amesema kuwa Baraza limeweza kutekeleza na kusimamia Shughuli nyingi kupitia ushauri wake na miongozo yake ikiwa ni kuboresha utendaji kazi na ufanisi kwa maendeleo ya Chuo.

Akitoa neno la shukrani, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo upande wa Taaluma, Utafiti na Ushauri wa kitaalam, Prof. Maulid Mwatawala amemshukuru sana Mkuu wa Chuo kwa uongozi wake mzuri na kuahidi kuyatekeleza yote aliyoyashauri ikiwemo kujiandaa kupambana na mapinduzi ya nne ya viwanda nchini.

“Tunakushukuru sana kwa kuhakikisha haya yote yametokea ndani ya miaka mitano ya uongozi wako, umekuwa sehemu ya uadilifu na umeifanya elimu ya SUA kuwa ya kujitegemea” alisema Prof. mwatawala

Mkutano huo kati ya Mkuu wa Chuo  na Wafanyakazi wote wa SUA uliambatana na Hafla fupi ya kumpongeza Jaji Warioba kwa kumpatia zawadi mbalimbali na kumtakia Heri Mkuu wa Chuo hicho kwa kumaliza miaka mitano ya awali ya uongozi wake tangu alipoteuliwa  mnamo mwezi Oktoba 2016 na kutegemea kuisha Novemba 2021.

Story and Photo Credits
Calvin Gwabara - SUAMEDIA

Share this page