Serikali yaipongeza SUA kwa tafiti nzuri za kilimo nchini

Serikali kupitia Wizara ya Kilimo imekishukuru Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa jitihada kubwa ambazo watafiti wake wanazifanya katika kufanya tafiti mbalimbali za kilimo zenye lengo la kusaidia kuboresha kilimo, kuinua maisha ya watanzania na kuinua pato la taifa.

SUA

Baaadhi ya wadau walioshiriki kwenye mkutano wa kupokea matokeo ya Tafiti kutoka APRA

Akizungumza  kwa niaba ya Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo,Mkurugenzi wa Sera na Mipango Wizara  ya Kilimo  Bwana Obadiah Nyagiro katika Warsha ya kitaifa ya kutoa mrejesho wa matokeo ya utafiti wa Mradi wa Utafiti wa Sera za Kilimo Barani Afrika (APRA) iliyofanyika Mkoani Dodoma tarehe 26 Oktoba 2021, amepongeza kazi kubwa iliyofanywa na watafiti kwenye mradi huo na hasa kitendo chao cha kuamua kurudisha matokeo ya utafiti wao kwa walengwa.

Mkurugenzi wa Sera na Mipango kutoka Wizara  ya Kilimo,  Bwana Obadiah Nyagiro akiwasilisha hotuba yake kwa wadau wa APRA

“Bila Utafiti hakuna jambo jipya lenye maamuzi ya kiserikali linaweza kutokea, kama kuna matamko yametoka bila utafiti utekelezaji wake hauwezi ukazaa mambo ambayo ni sahihi ambayo yanaweza yakaleta maendeleo kwa Wananchi, hivyo ni vizuri tafiti zifanyike na mabadiliko ya sera yafanyike kulingana na uchambuzi uliofanyika” amesema Bw Nyagiro.

Aidha Bwana Nyagiro ameeleza kuwa mipango ya Serikali hivi sasa inahimiza  Kilimo cha zao la Alizeti nchini ili kupunguza uhaba wa upatikanaji wa mafuta ya kula na kwa mwaka huu, Serikali imedhamiria kusisitiza kuongeza Kilimo cha Alizeti katika mikoa ya Dodoma na Singida na inaongeza   bajeti ya utafiti kwa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI) na kuwezesha wakala wa mbegu nchini (ASA) ili  kusaidia upatikanaji wa mbegu bora za Alizeti.

Katika hatua nyingine, Mkurugenzi huyo wa Sera na Mipango Wizara  ya Kilimo amesema zao la mpunga ni muhimu kwa usalama wa chakula, hivyo serikali inaedelea kuhimiza sekta binafsi kushirikiana na serikali kuwekeza katika miundombinu ya umwagiliaji ili uzalishaji wa mpunga ufanyike angalau mara mbili kwa mwaka.

Mtafiti kutoka katika Chuo Kikuu Cha Sokoine cha Kilimo SUA  Profesa John Jeckonia akitoa ufafanuzi kwa wanahabari kuhusiana na matokeo ya tafiti huo

Akielezea matokeo ya tafiti hizo, Mtafiti wa Utafiti huo  kutoka (SUA) Prof John Jeckonia amesema kuwa matokeo makubwa ambayo mradi huo umebaini ni kuwa kilimo cha  Alizeti kimeleta mchango mkubwa katika kupunguza umasikini kwa kuongeza vipato vya watu.

Amesema fursa mpya zimeibuka  kutokana na kilimo hicho na kwamba wapo waliopata manufaa kutoka katika kilimo hicho cha Alizeti kwa kuanzisha shughuli nyingine za kiuchumi ambazo pia zinamanufaa makubwa kwa maisha yao.

“ili kuondoa changamoto zilizopo, kuna mambo kadhaa yanatakiwa kufanyika, kwanza ni kuongeza huduma za ugani, upatikanaji wa pembejeo za kisasa, kuwahakikishia wakulima wanapata masoko ya bidhaa zao kwakuwa soko na bei ndo kitu kinachowavutia wakulima kuzalisha zaidi kwakuwa wakiwa na uhakika wa kuuza kwa bei bora wanaweza wakavutiwa zaidi kutumia mbegu za kisasa ambazo ni ghali kulinganisha na mbegu za kienyeji lakini ambazo uzalishaji wake kwa tija ni mkubwa na ni mzuri “alifafanua  Profesa Jeckonia.

Kwa upande mwingine, Mtafiti na Kiongozi wa Mradi wa APRA, Profesa Aida Isinika kutoka SUA ameomba Baraza la taifa la usimamizi wa mazingira (NEMC) kufuatilia ili kuhakikisha mazingira yanakuwa salama katika Wilaya ya Kilombero kutokana na matumizi mabaya ya viuatilifu hasa viua magugu yanayofanywa na wakulima  ambayo yasipodhibitiwa yanaweza kuleta athari kwa afya zao na mazingira pia.

“Matumizi ya viua magugu yanawasaidia kupunguza kazi lakini matumizi yale yanatumika kwa njia ambayo si sahihi kwa hiyo inawezekana huko mbele tukapata matatizo makubwa” alieleza Profesa Isinika.



Mkuu wa Mradi wa APRA na Mtafiti kutoka Chuo Kikuu Cha Sokoine cha Kilimo SUA Profesa Aida Isinika akiwasilisha matokeo ya tafiti kwa wadau

Aliongeza ”si hivyo tu, kupanuka kwa Mashamba ya mpunga kuna athari kwenye mabwawa yanayotumika kutengeneza umeme hivyo tunaweza tukapanua lakini tukawa na madhara ya kufanya uharibifu kule  hivyo hayo ni mambo yanayotakiwa kufanyiwa kazi”.

Utafiti huo umefanyika tangu mwaka 2017 na unategemewa kukamilika mapema mwakani na tayari umeshafanyika katika nchi sita ambazo ni Tanzania, Ethopia, Malawi, Zimbabwe, Ghana na Nigeria kwakujikita kuchambua mmbo ya kisera yanayowezesha au kuhamasisha kilimo endelevu na shirikishi.

Hizo zote ni kujuhudi za kuboresha Maisha ya wadau katika minyororo ya thamani ya kilimo ambapo kwa hapa Tanzania utafiti huu uliratibiwa na watafiti kutoka Chuo Kikuu Cha Sokoine cha Kilimo SUA  katika wilaya ya Kilombero wakijikita katika zao la mpunga na wilaya za ikalama na Iramba kwa zao la Alizeti



Mtafiti kutoka Chuo Kikuu Cha Sokoine cha Kilimo SUA Profesa Mtengua Mdoe akichangia jambo kwenye kikao

Dkt. Christopher Magomba Mhadhiri na Mtafiti katika mradi huo  kutoka Chuo Kikuu Cha Sokoine cha Kilimo SUA  akitoa maelekezo mafupi kuhusiana na tafiti

Wadau wakifatilia wasilisho la matokeo ya tafiti wa APRA

Story and Photo Credits
Amina Hezron - SUAMEDIA

 

Share this page