Marekani kushirikiana na SUA kuinua, kuimarisha sekta ya kilimo

Balozi wa Marekani nchini Tanzania Dkt. Donald J. Wright, amesema Marekani itaendelea kuimarisha ushirikiano na Tanzania katika kuinua na kuimarisha sekta ya Kilimo kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Sokoine cha kilimo SUA kwa kufanya tafiti za kilimo, kutoa elimu na uvumbuzi. 

SUA

Balozi wa Marekani nchini Tanzania Bw. Donald J Wright akizungumza wakati wa Maadhimisho ya miaka 60 ya ushirikiano wa kidiplomasia baina ya nchi ya Tanzania na Ubalozi wa Marekani

Ameyasema hayo Novemba 16, 2021 kwenye maadhimisho ya miaka 60 ya uhusiano wa kidiplomasia baina ya nchi ya Tanzania na Ubalozi wa Marekani uliofanyika ukumbi wa Multipurpose kampasi ya Edward Moringe SUA.

Balozi Dkt. Wright amesema kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita Serikali yao kupitia shirika la Marekani la maendeleo ya kimataifa USAID lilitumia dola milioni 200 katika mradi wa feed the future ambao umewanufaisha wakulima zaidi ya 700,000, kukuza sekta ya kilimo na  wazalishaji wengine wa chakula.

Aidha amesema kuwa Serikali yao imelenga kuchangia asilimia 20 kupunguza umasikini kwa Tanzania na nchi zingine lengwa kwa kipindi cha miaka mitano ijayo, na kuongeza kuwa katika hatua hiyo Rais wa nchi hiyo Joe Biden ameidhinisha bajeti ya kiasi cha dola billion 5 ya mpango huo.

Awali akizungumza kwa niaba ya Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha kilimo Prof. Raphael Chibunda Naibu Makamu mkuu wa Chuo upande wa Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalam Prof. Maulid Mwatawala, amesema ushirikiano huo umeiwezesha SUA kupata miradi zaidi ya 30 yenye kufikia thamani ya  dola  milioni 58 pamoja na programu mbalimbali zilizofundishwa Chuoni hapo.

“Wasomi wengi Tanzania wameweza kupata fursa ya kusoma nchini marekani na nchi zingine zilizoendelea hakika ushirikiano huu umesaidia kutoa fursa kwa vijana wetu na umeongeza ukuaji kiuchumi nchini kupitia hili .tunajivunia sana“ alisema Prof. Mwatawala 

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Mhe. Halima Okash amesema serikali inahitaji kutumia wasomi kutoka SUA kutafuta utatuzi wa changamoto zinazowakumba wakulima wa Tanzania ikiwemo magonjwa ya mazao, wadudu shambulizi na mabadiliko ya Tabia nchi.

“sisi kama Serikali tunafarijika sana kwa uhusiano huu kati ya Chuo cha SUA na Ubalozi wa Marekani ukweli tunawaunga mkono pia tunamatumaini makubwa kwenu katika kupata uvumbuzi wa mambo mbalimbali yanayohusu kilimo hasa kuwasaidia wakulima wetu nchini’’ alisema Mhe. Halima

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti na Kupunguza Umaskini Tanzania (REPOA), Dkt. Donald Mmari alisema Serikali ya Marekani imekuwa na  uhusiano  mkubwa na   Chuo Kikuu cha SUA  tangu mwaka 1962 kilipokuwa Kitivo cha Kilimo cha Chuo Kikuu Dar es Salaam kupitia shirika la maendeleo USAID kiliwezesha kiasi cha fedha katika uwanzishwaji wake .

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti na Kupunguza Umaskini Tanzania (REPOA), Dkt. Donald Mmari

Alisema kuwa uhusiano huo umelenga hasa katika kubadilisha sekta ya kilimo kutoka katika matumizi duni ya Teknolojia na uzalishaji pia kufanya kilimo kiwe cha kisasa na hasa kuwaingiza vijana katika uzalishaji wa sekta kilimo nchini.

“Nchi yetu ina vijana walio wengi na rasilimali za kilimo tulizonazo ni nyingi lakini hazijatumiwa vizuri hivyo ni lazima tuangalie namna ya kuwaongezea vijana wetu ujuzi na stadi mbalimbali wawe wazalishaji bora ili waweze kubadilisha mfumo wa kilimo chetu” alisema Dkt. Mmari
 

Share this page