Kilimo Ikolojia ni msaada mkubwa kwa wakulima

Imebainishwa kuwa Wakulima wengi nchini hawana uwezo wa kumudu gharama za kununua madawa na mbolea kwaajili ya kustawisha mashamba na kuua wadudu na magonjwa kwenye mazao yao hivyo Kilimo Ikolojia kinaweza kuwa msaada mkubwa kwa wakulima.

SUA

Waziri wa Kilimo,Umwagiliaji na mifugo  wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe. Soud Hassan akifunga Kongamano hilo la Kitaifa la Pili la Kilimo Hai

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Kilimo,Umwagiliaji na mifugo  wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe. Soud Hassan kwa niaba ya Waziri wa Kilimo Mhe. Profesa Adolf Mkenda wakati akifunga Kongamano la Pili la kitaifa la Kilimo Hai lililofanyika kwa siku mbili ( 22 - 23 Oktoba 2021) Jijini Dodoma na kuwakutanisha wadau wote wa Kilimo Hai kutoka ndani na nje ya Tanzania.

“Niwatake wadau wote wa kilimo Hai nchini kuhakikisha malighafi zinazozalishwa za kuulia wadudu na magonjwa pamoja na mbolea ziweze kupatikana kwa wingi, kwa urahisi na kwa bei nzuri kwenye maeneo mbalimbali nchini ili ziweze kuwafanya wakulima wetu waachane na matumizi makubwa ya madawa na mbolea za viwandani” Alisema Mhe.Waziri.

Amewahakikishia kuwa Serikali ya Tanzania iko pamoja na wadau wote wa kilimo Hai na imeiweka katika mipango yake na ili kuendana na mabadiliko ya tabia nchi mbegu stahimilivukwa uhakikika wa chakula lishe na kuongeza kipato zinahitajika.

Mhe. Waziri huyo wa Kilimo Zanzibar amesema serikali sikivu ya Tanzania imetengeneza mazingira Rafiki ya kilimo Hai kupitia sera yake ya kilimo ya mwaka 2013 na inatambua mchango wa utafiti wa kilimo Hai kupitia wanafunzi wa Shahada za Uzamili na uzamivu wa Chuo kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA.

“Malengo makubwa ya Wizara ya kilimo ni Utafiti,Tija ya uzalishaji,Upatikanaji wa Pembejeo husasani mbolea viutilifu,mbegu bora na zana za Kilimo,Masoko ya mazao,Uongezaji thamani wa mazao na Miundombinu ya umwagiliaji” Alisisitiza Mhe. Hassan.

Aidha amesema Tanzania ina wakulima wa Kilimo Hai waliosajiliwa wanafikia wakulima 600,000 na kwa idadi hiyo kubwa ni vyema TOAM kuendelea kuwatambua na kuwasajili ili kuendelea kuwatumia kwa lengo la kuzalisha chakula.



Profesa Benard Chove akitoa salamu za Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA kwa niaba ya Makamu Mkuu wa chou hicho Profesa. Raphael Chibunda

Akitoa salamu za Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA Prof. Benard Chove kwa niaba ya Makamu Mkuu wa chuo Prof. Raphael Chibunda amesema jukumu la SUA ni kuchangia katika maendeleo ya nchi kwa kufanya mafunzo,Kufanya Utafiti na kutoa huduma kwa jamii.

”Ni matumaini yangu washiriki kutoka SUA wameweza kutoa maelezo kuhusu shughuli mbalimbali zilizofanyika na zinazoendea kufanyika katika kuhakikisha Chuo kinatoa mchango wake katika kuendeleza Kilimo ikolojia kupitia mafunzo utafiti na ushauri,Alibainisha Profesa Chove.

Prof. Chove amesema kuwa Chuo kimeendelea kuyaishi maono na malengo na maagizo ya Baba wa Taifa ya kuanzisha Chuo hicho na kusema kuwa matunda yake yamekuwa ni uwepo wa idadi kubwa ya wataalam bora kwenye Nyanja zote za Kilimo wanaozalishwa Chuoni hapo kila mwaka.

Ameedelea kusema kuwa yote ambayo SUA imeyatekeleza kwa kipindi chote hicho toka kuanzishwa kwake juu ya mafunzo na kuchangia katika maendeleo ya Kilimo Ikolojia yasingeweza kufanyika bila ushirikiano ambao wameupata kutoka kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wadau mbalimbali wa maendeeo.

“Hivyo napenda kuwashukuru wadau wetu wa maendeleo kama vile Serikali ya Denmark kupitia mradi wa BSU,SWISSAID,Wakfu wa Mcknight kutoka Marekani,Shirika la Maendeleo la Ubelgiji na Asasi zingine zisizo za Kiserikali na wengine wengi. Aidha napenda kuchukua nafasi hii kuwahakikishia kwamba Chuo kitaendela kutoa ushirikiano na kufanya kila linalowezekana katika kuhakikisha malengo ya ushirikiano wetu yanafanikiwa kwa manufaa ya watanzania wote na Taifa kwa ujumla” Alisema Prof. Chove

Profesa Chove amesema miongoni mwa mafanikio ya ushirikiano na wadau hao ni kuanzisha Shahada ya Uzamivu ya Kilimo Ikolojia ambayo imeingia mwaka wa pili lakini mandalizi ya kuanzisha Shahada ya umahiri ya Kilimo Ikolojia nayo yanaendelea na hii itasaidia kuboresha na kujenga uwezo zaidi kwa Chuo katika kutoa huduma kwa jamii.

Waziri wa Kilimo,Umwagiliaji na mifugo  wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe. Soud Hassan (katikati) akimkabidhi cheti cha pongezi kwa kufanisha Mkutano huo mkubwa Profesa Benard Chove kwa niaba ya SUA

Picha ya pamoja ya washiriki kutoka SUA wakiwa wameambatana na wakulima kutoka maeneo mbalimbali ambao wanafanya tafiti na kushiriki kwenye miradi mbalimbali ya kilimo Hai inayotekelezwa na SUA


Washiriki wa mkutano huo wakifuatilia hotuba za ufungaji wa mkutano huo wa pili wa kitaifa wa Kilimo Hai

Washiriki wa mkutano huo wakifuatilia hotuba za ufungaji wa mkutano huo wa pili wa kitaifa wa Kilimo Hai

STORY & PHOTO CREDITS

Calvin Gwabara - SUAMEDIA

Share this page